CHAMA CHA WANAWAKE WANASHERIA TANZANIA TAWLA CHAZINDUA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 25 TANGU KIANZISHWE
4:07 PM
By
Ujamaa Orphanage Foundation
0
comments
CHAMA cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA) kwa kipindi cha miaka 25 kimetoa msaada wa kisheria kwa wanawake milioni tano katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Arusha na Dodoma.
Hayo yalielezwa na Makamu Mwenyekiti wa Balaza la TAWLA, Margareth Ringo wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana katika maadhimisho ya miaka 25 ya kujengea uwezo na kufanya uchechemuzi juu ya haki ya wanawake.
“TAWLA inajivunia mafanikio makubwa iliyopata ndani ya kipindi cha miaka 25 kimeweza kutoa msaada wa kisheria kwa wanawake wasiopungua milioni tano kupitia vituo vilivyopo Dar es Salaam, Tanga,Arusha na Dodoma” alisema Ringo.
Alisema pia wameweza kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa kutumia simu bila malipo kupitia namba 08007510101/0800110017.
Ringo aliongeza kuwa katika kuhakikisha jamii za pembezoni zinaweza kuifikia haki TAWLA imetoa mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria 402 katika wilaya 18 Tanzania ambazo ni Bahi, Kongwa, Mpwapwa, Chamwino, Mpanda vijijini, Mpanda Mjini, Arumeru, Longido, Monduli, Arusha, Karatu, Muheza, Tanga, Kisarawe, Mvomero, Ilemela Magu na Ilala.
Alisema wasaidizi hao wamesaidia kuwafikia zaidi ya watu 10,500 waliokuwa na matatizo ya kisheria na pia namba kubwa zaidi wameweza kupata elimu ya maswala ya kisheria.
Aliongeza kuwa pamoja na kutoa msaada wa kisheri wameweza kuihamasisha jamii juu ya masuala ya kisheria kupitia machapisho mbalimbali na vyombo vya habari na michezo ya kuigiza ambapo watu zaidi ya milioni 15 wamefikiwa.
Alisema chama hicho kimekuwa kikishiriki kutetea mabadiliko ya sheria kandamizi kwa wanawake na za kuwalinda, mchakato wa kupitisha kwa sheria ya mtoto na sheria ya makosa ya kujamiana, kuchangia uteuzi na ushiriki wa wanawake kwenye vyombo vya maamuzi na kuwa chama hicho kina mahusiano mazuri na wadau mbalimbali wakiwemo asasi zisizo za kiserikali, serikali kuu na za mitaa.
Ringo alisema katika kusherehekea mafanikio ya miaka 25 TAWLA kuanzia Mei 10 hadi 29 wanatakuwa na shughuli mbalimbali za uhamasishaji wa kuandika wosia na utaenda pamoja na uandikishaji wosia bila gharama kwa wale ambao watakuwa tayari katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Arusha na Dodoma pamoja na kutoa msaada wa kisheria katika baadhi ya mikoa.
(Imeandaliwa na mtandao wa http://www.habarizajamii.com/
0 comments: